Tarehe: 16/11/2016.
TAARIFA YA HABARI RADIO HURUMA

HABARI ZA TANGA:

VIJANA MKOANI TANGA WATAKIWA KUJITUMA KATIKA KAZI.
Vijana wa mkoa wa Tanga wametakiwa kijituma katika kazi ili waweze kujitafutia maendeleo kwani maendeleo yanaletwa na kijana wenyewe na sio serikari. Yamesemwa na Yusuph Bakari ambaye ni wakala wa simu katika eneo la Ngamiani kati kwani licha ya kuwa mlemavu wa viungo ameweza kujiajiri mwenyewe na anategemewa na jamii yake, licha ya hali aliyonayo. Pia amesema baadhi ya vijana wengi mkoani hapa wanao uwezo wa kuanzisha miradi midogo midogo lakini hawako tayari na wameamua kujikita katika makundi maovu yakiwemo uvutaji bangi, ulevi, pamoja na ujambazi. Aidha mfanyabiashara huyo ameweza kushauri vijana pamoja na jamii kwa ujumla na kufafanua zipo athari ambazo ni rahisi kuzipata pale wanaposhindwa kujituma.

WAJUMBE KUTOKA ZANZIBAR WATEMBELEA BANDARI YA TANGA.
WAJUMBE wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi Baraza la Uwakilishi la Zanzibar wametembelea bandari ya Tanga eneo la upakuaji wa shehena ya mizigo na kutazama fulsa za ujio wa Mradi wa Bomba la Mafuta Mkoani Tanga. Wajumbe hao 14 wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma walitembelea eneo itakapojengwa bandari mpya ya Mwambani Tanga wamesema fulsa hizi zitaongeza ajira kwa vijana wakiwemo Wanzanzibar waishio Tanga. Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Hassan amesema Serikali ya Zanzibar imejipanga kuimarisha bandari zake ikiwemo ya Wete na Mkoani Kisiwani Pemba ikiwa ni maandalizi ya ujio wa Bomba la Mafuta. Akizungumzia kilio cha wafanyabiashara na wasafiri wa Pemba na Tanga kwa kutumia usafiri wa baharini, Hassan amesema kero hiyo Serikali inaitambua na jitihada za kuwa na meli ya uhakika inafanywa. Amesema baadhi ya wafanyabiashara wa Pemba ambao walikuwa wakichukua bidhaa Tanga wamekatisha na baadhi yao mitaji kufa kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa baharini. Awali akizungumza na wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi, Kaimu Meneja wa Badari Tanga, Henry Arika, amesema mchakato wa mradi wa bomba la mafuta unaenda kwa kasi na kuwataka wawekezaji kutoka Zanzibar kuja kuwekeza. Arika amesema Tanga ziko fursa nyingi za uwekezaji na yako maeneo mengi hivyo kupitia ujio wa mradi wa Bomba la mafuta amewataka wawekezaji wa ndani kuchangamkia fulsa zilizopo.

POLISI ATAFUTWA NA JESHI LA POLISI TANGA KWA MAUAJI YA MWENZAKE.
.JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linamsaka askari wa jeshi hilo, Michael Komba kwa tuhuma za kumpiga askari mwenzake wa kike hadi kumsababishia kifo. Taarifa zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Mngambugha, zinamtaja marehemu kuwa ni polisi Elizabeth Stefano wa Kituo cha Polisi Kati, Chumbageni, jijini Tanga. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:00 usiku wa kuamkia juzi, eneo la Sahare jijini Tanga ambako ni nyumbani kwa marehemu. Wakizungumza kwa sharti la kutoandikwa majina yao baadhi ya majirani walidai kuwa chanzo cha ugomvi huo kinadhaniwa kuwa ni wivu wa mapenzi, wakidai kwamba Komba alikuwa akimtuhumu Elizabeth kutokuwa mwaminifu katika uhusiano wao.


HABARI ZA KITAIFA:

MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA APEWA MWEZI MMOJA KUFANYA MABADILIKO.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika hilo ili kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi. Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka kutoa huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora ya ndege barani Afrika. Waziri Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa Shirika hilo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za kulifufua na kuliimarisha Shirika hilo. Pia Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo kuzunguka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL. Ameongeza kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo katika mashirika ya ndege nchini. Profesa Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa kukata tiketi kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa shirika hilo kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.

SERIKALI YAIAGIZA IDARA YA UHAMAJI TANZANIA KUHAKIKI UPYA VIBALI VYA WAHAMIAJI WOTE NCHINI.
SERIKALI imeagiza idara ya uhamiaji nchini kufanya uhakiki upya wa vibali vya wahamiaji wote walioko nchini na kwa wale ambao hawana sifa zinazostahili warudishwe kwenye nchi zao kwakuwa wanaishi nchini kinyume na sheria za nchi zinavyoelekeza. Agizo hilo limetolewa jana na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba alipokutana na viongozi wa idara ya uhamiaji nchini kwaajili ya kujadili na kutatua kero mbalimbali katika idara hiyo. Kwa upande wa mifumo ya utoaji vibali Mwigulu ameiagiza idara hiyo iunde tume maalum ya kujadili nakuangalia namna ya kuweka mifumo maalum ya kutoa vibali vya uraia kwa urahisi ili kupunguza malalamiko na ufisadi ambao kama hautatatuliwa mapema utasababisha hasara kwa taifa. Aidha aliwaagiza watawala katika idara hiyo kutenda haki kwa watumishi wake na watanzania kwa ujumla sambamba na kuwalipa madeni yao watumishi wapya walioajiriwa na idara ya uamiaji nchini.


WENYEVITI NA WATENDAJI WA VIJIJI NA KATA ZA MKOANI PWANI, WAONYWA KUUZA ARDHI ZA VIJIJI KWA MASLAHI YAO.
MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amewataka baadhi ya watendaji na wenyeviti wa vijiji na kata kuacha kujihusisha na uuzaji wa ardhi za vijiji na maeneo ya wawekezaji ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima. Aidha amesema wapo baadhi ya viongozi hao ambao wanageuza ardhi hizo kutunisha mifuko yao hali inayosababisha serikali za vijiji kukosa mapato. Hayo ameyasema kwa wananchi wa kata ya Soga ,Kibaha Vijijini,baada ya kutembelea mipaka ya eneo la ardhi ya mwekezaji Mohammed Interprises ,ambalo lina mgogoro na wananchi hao. Mhandisi Ndikilo, ameeleza kuwa kuna taarifa kuwa wapo wenyeviti na watendaji wa vijiji wanaozuza ardhi za vijiji hekari zaidi ya 50 zinazotakiwa kisheria na kuuza hadi hekari 100-300. Amefafanua kwamba anafanya uchunguzi na endapo yupo atakaebainika kuuza ardhi kiholela hatoweza kumvumilia na sheria itafuata mkondo wake. Amesema inashangaza kuona kiongozi badala ya kusimamia masuala ya serikali ndio ana kuwa chanzo cha kuchonganisha migogoro kwenye jamii. Nae mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini , Hamoud Jumaa ,amesema anashirikiana vizuri na mkuu wa mkoa, na wa wilaya juu ya tatizo la mwekezaji huyo na wananchi. Vile vile amewaomba wananchi wajenge tabia ya kusikiliza viongozi na kujenga tabia ya kuepukana na migogoro inayochelewesha muda wa kufanya mambo mengine ya kimaendeleo na isiyo na manufaa.


HABARI ZA KIMATAIFA:

WATU LAKI 8.5 WAENDELA NA MAISHA YA UKIMBIZI, JAMHURI YA AFRIKA YA KATI.
SHIRIKA la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema zaidi ya watu laki 8.5 nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, nusu yao wakiwa watoto, wanaendelea na maisha ya ukimbizi wa ndani au katika nchi za jirani, kutokana na kutokuwa na usalama baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2012. Maofisa wa mashirika ya misaada wanatarajiwa kukutana kesho huko Brussels kujadili mchakato wa ufufuaji wa uchumi wa Jamhuri ya Afrika ya kati, na kukusanya fedha kwa ajili ya mpango wa misaada kwa nchi hiyo.

WATALII MILIONI 4 WATEMBELEA MISRI TANGU KUANZA MWAKA 2016.
WAZIRI wa utalii wa Misri Yehia Rashed amesema watalii wapatao milioni 4 wametembelea Misri mwaka huu, wakiwemo milioni 1.5 kutoka nchi za kiarabu. Amesisitiza kuwa watalii kutoka nchi za kiarabu ni muhimu kwa sekta ya utalii nchini Msiri, kutokana na ukaribu wa kijiografia. Sekta ya utalii inayoajiri watu milioni 4 nchini humo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya taifa na fedha za kigeni, ambayo mwaka 2010 pekee iliiletea Misri pato la dola za kimarekani bilioni 13.

NIGERIA YAKUMBWA NA NJAA KALI.
Umoja wa Mataifa umetoa tamko kwamba wanaijeria wapatao nilioni kumi na nne wanahitaji misaada ya kibinaadamu upande wa Kaskazini mwa nchi hiyo, mahali ambako maelfu kwa mamia ya watoto wako kwenye hatari kubwa ya kifo kutokana na njaa kali na kwamba watoto laki nne wanahitaji msaada wa dharula. Inaelezwa kuwa mkoa uliokumbwa na baa hilo la njaa awali ilikuwa ngome ya zamani ya kundi la dola ya kiislamu Kiislam, Boko Haram.Jimbo hilo lilikuwa katika hali tete kiasi cha kutokufikiwa na misaada ya kibinaadamu kwa miaka kadhaa sasa ambapo kwa sasa ndiyo limebainika kuwa na hali mbaya ya chakula na njaa kali ikiwemo majimbo ya Borno,Yobe na Adamawa. Shirika la kuwasaidia watoto la , Unicef, limesema kwamba inakadiwa kuwa watoto wapatao elfu sabini na watano wako katika hatari ya kufa. Mapema , shirika la misaada ya kitabibu la madaktari wasio kuwa na mipaka wamegundua idadi kubwa zaidi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika kambi mbili za wakimbizi utafiti ambao uliainishwa kwa kiasi kikubwa kuwa wa chini kuliko ilivyotarajiwa, na kwamba inaaminika robo ya watoto hao walikwisha kufa